Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kimehadharisha walaji wa nyama ya nguruwe nchini, kuwa wanakabiliwa na
hatari ya kupata kifafa.
Utafiti wa kisayansi uliofanywa na SUA,
umebaini kuwa baadhi ya nguruwe wana minyoo aina ya tegu ambao nyama yao
ikiliwa bila kuiva vizuri, mlaji atapata minyoo hiyo ambayo huingia
kichwani na kusababisha kifafa.
Akizungumza na mwandishi hivi karibuni,
Mhadhiri na Mtafiti wa Idara ya Sayansi ya Wanyama na Uzalishaji ya SUA,
Profesa Faustine Lekule, alisema sampuli za utafiti huo kutoka Mbeya,
zimebaini nguruwe wengi wakiwamo wanaosafirishwa katika miji mikubwa
wameathirika na minyoo hiyo.
Kwa mujibu wa Profesa Lekule, wataalamu
wa SUA wanaosimamia Mradi wa Utafiti wa Kuboresha Ufugaji wa nguruwe kwa
mkoa wa Mbeya ili kuinua pato la kaya, unaofadhiliwa na Shirika la
Kimataifa la Maendeleo la Denmark (DANIDA), walibaini hatari hiyo baada
ya kuchukua sampuli ya nyama ya nguruwe kwa ajili ya vipimo.
“Majibu ya sampuli ambazo wataalamu
wamezichukua kutoka kwa nguruwe wa wafugaji kwenye baadhi ya vijiji,
wamebainika kukumbwa na hatari hii.
“Lazima jitihada za makusudi zichukuliwe
katika kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa tatizo hili kati ya watafiti na
Serikali,” alisema Profesa Lekule.
Alisema maambukizi ya tegu au minyoo ya
nguruwe yanatokana na tabia za baadhi ya wafugaji kutozingatia ufugaji
bora kwa kuwaacha kujitafutia chakula na maji mitaani na kula kinyesi
cha binadamu.
Kwa mujibu wa Profesa Lekule, baadhi ya
wafugaji wamekuwa wakijisaidia vichakani na kuwaacha nguruwe kutafuta
malisho katika vichaka na kula kinyesi chao, hali inayochangia ongezeko
la maambukizi ya minyoo ya tegu hao.
Baada ya kula kinyesi minyoo humwingia
mwilini na kumdhoofisha na baadaye binadamu anapokula nyama ambayo
haijaiva vizuri, minyoo hiyo humwingia na kusababisha kifafa baada ya
kuingia kichwani.
Alisema athari za kuenea kwa maambuziki
hayo inaweza kutokea katika miji mikubwa ikiwamo Dar es Salaam kwa kuwa
nguruwe wa Mbeya husafirishwa na kuuzwa maeneo hayo.
“Hatua hii inaweza kusababisha kusambaa
kwa ugonjwa huu, hivyo ushirikiano kati ya wafugaji, wafanyabiashara,
Serikali na wataalamu wa afya katika kufikia hatua ya kumaliza
changamoto hii unahitajika,” alibainisha Profesa Lekule
No comments:
Post a Comment