Picha ya mtotot wa kiume mwenye umri wa miaka 13 |
Tatizo
la kuota matiti kwa wanaume na watoto limekuwa kubwa sana katika dunia
ya leo. Inawezekana kabisa wakati unatembea njiani ukaona wanaume au
watoto wadogo wa kiume wakiwa na matiti makubwa ambapo watu wengi
huchukulia kama ni kawaida. Kitaalamu gynecomastia ni kukuwa kuliko
kawaida yake kwa tishu ya kwenye titi inayojulikana kama glandular
tissue. Tatizo hili huonekana sana kwa watoto wachanga na wanaume
waliokatika umri wa kubaleghe, lakini pia huonekana kwa watu wazima na
wazee.
Ukubwa wa tatizo (epidemiology)
Asilimia
60-90 ya watoto wachanga wanapata tatizo hili la kukuwa kwa matiti kwa
mpito linalojulikana kitaalamu kama transient gynecomastia kutokana na
kuwepo kwa kichocheo cha aina ya estrogen kwa wingi wakati wa ujauzito
wa mama.
Kati
ya asilimia 4-69 ya vijana walio katika umri wa kubaleghe imeonekana
wanapata tatizo hili kutokana na kuwepo kwa wingi kwa kimengenyo aina
ya estradiol.Mara nyingi huonekana katika umri kati ya miaka 10-12 na
hupotea taratibu ndani ya miezi 18, si kawaida yake kuonekana kwa
vijana walio na umri ya zaidi ya miaka 17. Asilimia 24-65 ya watu
wazima hupatwa na tatizo hili, hii hutokana na kubadilishwa kwa wingi
kwa kichocheo aina ya testerone kuwa estradiol na kutolewa kwa uchache
kwa kichocheo hiki cha testerone kutoka kwenye korodani zinazoanza
kuzeeka..Ikumbukwe ya kwamba kichocheo hiki testerone hutengenezwa
katika korodani za mwanamume.
Pathofiziolojia (Nini hutokea?)
Kuongezeka
ukubwa wa matiti kwa wanaume hutokana na kuharibika kwa mfumo wa
vichocheo unaojulikana kama estrogen-androgen balance na hivyo
kusababisha estrogen kutolewa kwa wingi ama kuongezeka kwa msisimko
(sensitivity) wa matiti kwa kiwango cha zaidi ya kawaida kwa kichocheo
aina ya estrogen kilicho kwenye mzunguko wa damu.Estrogen husababisha
chembechembe zinazojulikana kama ductal epithelia kuongezeka kwa wingi,
kurefuka (ductal elongation) na kugawanyika, kuongezeka kwa
chembechembe za mafuta (ductal fibroblasts) na kuongezeka kwa mfumo wa
damu kwenye matiti (increase vascularity).Estrogen hutengenezwa kutoka
kwenye vichocheo vya testerone na androgen kwa kutumia kimengenyo
kinachojulikana kama aromatase.
Aina za gynecomastia
•Puffy nipples – Kuongezeka ukubwa wa chuchu za matiti kutokana na kuongezeka kwa tishu aina ya glandular tissue.
•Pure
glandular gynecomastia – Huonekana sana kwa wale wanaofanya mazoezi ya
kujenga mwili (bodybuilders), kutokana na matumizi ya dawa za kujenga
mwili (anabolic steroids) ambazo zinakuwa na kiwango kikubwa cha
kichocheo aina ya testerone, ambacho hubadilishwa kuwa estrogen. Kwa
wanaume wembamba, tatizo hili hutokea kutokana na kuongezeka kwa breast
tissue gland pamoja na kuwepo/kutokuwepo kwa tishu aina ya adipose
tissue.
Ni nani aliyekatika hatari ya kupata tatizo hili?
•Wanaume walio na umri zaidi ya miaka 50.
•Wenye uzito uliopitiliza (Obesity)
•Unywaji pombe kupindukia
•Magonjwa sugu ya figo au ya Ini
•Kuwepo kwa historia ya tatizo hili katika familia.
Visababishi vya kukuwa kwa matiti kwa wanaume
•Pseudogynecomastia
– Kuongezeka kwa tishu zinazozunguka chuchu za matiti na huambatana na
kuwepo kwa wingi wa tishu aina ya adipose. Mazoezi na kula vyakula
venye virutubisho sahihi huondosha tatizo hili.
•Unilateral/asymetrical
gynecomastia – Ni kuongezeka kwa titi moja pekee au la upande mmoja wa
mwili wa mwanamume kutokana na sababu mbalimbali. Titi la upande wa
pili huwa kwenye umbile na saizi ya kawaida. Bilateral gynecomastia
ni kuongezeka kwa matiti yote mawili.
•Hypogonadism
– Kutofanya kazi kwa korodani vizuri na kuwa ndogo. Hii husababishwa
na magonjwa mbalimbali kama klinifelter'rs syndrome, pitituary
insuffiency na nk.
•Umri
– Kuzeeka pia kumehusishwa kutokea kwa tatizo hili kutokana na
kutolewa kwa uchache kwa kichocheo cha testerone na kuongezeka kwa
juhudi za kutengeneza kwa wingi kwa kimengenyo aina ya estradiol kutoka
kwenye kichocheo aina ya testerone. Pia mabadiliko ya mfumo mzima wa
vichocheo mwilini hasa kwa wale wenye uzito uliopitiliza.
•Uzito
uliopitiliza (Obesity) – Watu wenye uzito uliopitiliza hupatwa na
tatizo hili kutokana na kuharibika kwa mfumo wa vichocheo mwilini na
hivyo kuongezeka kwa kichocheo aina ya estrogen mwilini mwao na wakati
huohuo kupungua kwa kichocheo kingine aina ya testerone.
•Saratani
– Baadhi ya saratani kama saratani ya kwenye korodani, kwenye tezi
lililojuu ya figo (adrenal gland), saratani ya tezi la kichwa
(pitituary tumor), huharibu mfumo mzima wa vichocheo mwilini hasa wa
kuweka sawa vichocheo kati ya uanaume na uanawake (male-female hormonal
balance).
•Hyperthyroidism – Kukuwa kwa ukubwa wa tezi la koo (thyroid gland) na hivyo kutengeneza kwa wingi kichocheo aina ya thyroxine.
•
Tatizo la figo kushindwa kufanya kazi (Renal/Kidney failure) - Nusu ya
wagonjwa wote wanaotibiwa tatizo la figo kushindwa kufanya kazi kwa
kutumia hemodialysis hupatwa na tatizo hili la kukuwa kwa matiti
kutokana na kuharibika kwa mfumo wa vichocheo mwilini (hormonal
imbalance).
•Matatizo
ya Ini – Dawa za kutibu magonjwa ya kwenye Ini kama liver cirrhosis,
liver failure husababisha kutokea kwa tatizo hili kutokana na
kukosekana kwa uwiano sawa wa mfumo wa vichocheo mwilini.
•Utapia
mlo, ukame – Utapia mlo, ukame au kujikondesha husababisha kupungua
kwa kichocheo aina ya testerone na kuongezeka kwa kichocheo aina ya
estrogen na hivyo kuharibu mfumo wa vichocheo mwilini. Hii hutokana na
kukosekana kwa virutubisho sahihi mwilini ambavyo vingi husaidia
kurekebisha mfumo wa vichocheo mwilini na hivyo kumuepusha mtu na
magonjwa mbalimbali pamoja na tatizo hili.
•Madhara ya dawa za kurefusha maisha (Antiretroviral therapy) kwa wagonjwa wa ukimwi.
•Utumiaji wa madawa ya kulevya kama bangi/marijuana.
Vipimo vya Uchunguzi
Vipimo hivi vitafanywa kulingana na historia ya mgonjwa, dalili na viashiria vya mgonjwa baada ya kupimwa na daktari.
•Kipimo
cha damu (Complete Blood Count) – Kuangalia wingi wake, aina
mbalimbali za chembechembe za damu na uwepo wa maambukizi ya bakteria.
•X-ray
ya matiti (Mammogram) – Hutumiwa kuangalia tishu za kawaida na zile
ambazo si za kawaida zilizo kwenye matiti. Husaidia kugundua uwepo wa
saratani, cysts, na calcifications kwenye matiti.
•Liver
function test – Mjumuiko wa vipimo vya damu kuangalia aina mbalimbali
za vichocheo na vimengenyo ili kuweza kutambua kama mgonjwa ana ugonjwa
wowote ule wa Ini na chanzo chake, vipimo hivi huangalia albumin,
Alanine transaminase (ALT), Aspartate transaminase (AST), Alkaline
phosphatase (ALK), Total bilirubin (TBIL), Direct bilirubin (Conjugated
Bilirubin), Gamma Glutamyl Transpeptidase (GGT), Lactate
Dihydrogenase (LDH).
•Tumor markers – Kipimo cha damu cha kuangalia viashiria vya saratani ya korodani kama AFP alpha feto 1 protein, Beta-HCG, LDH.
•Kipimo
cha damu cha kuangalia wingi wa kichocheo cha aina ya testerone (Total
and Free Testerone) Hufanyika asubuhi ambapo kiwango cha testerone
huwa juu. Kiwango cha kawaida cha kichocheo cha testerone ni 300 - 1000
ng/dl (Kiwango hiki hupungua kwa asilimia 13 wakati wa mchana).
•Kipimo
cha damu cha kuangalia vichocheo vinavyoonekana kwenye ugonjwa wa
kukua ukubwa wa tezi la koo ( hyperthyroidism) kama kichocheo aina ya
Thyroid Stimulating Hormone (TSH) ambacho huwa katika kiwango kidogo
wakati wa kuugua ugonjwa wa hyperthyroidism, hutolewa na tezi la kwenye
kichwa aina ya pitituary gland, vichocheo vyengine aina ya anti-TSH
receptor antibodies (kwa wenye ugonjwa wa Grave’s disease),
anti-thyroid – peroxidase (kwa wenye ugonjwa wa Hashimoto’s disease),
na pia kuangalia wingi wa vichocheo aina ya T3 na T4. Kipimo cha
Thyroid Scintigraphy pia huweza kutumiwa kutofautisha kati ya ugonjwa
wa hyperthyroidism na ugonjwa wa thyroiditis. Kipimo hiki hutumia
madini ya mionzi ya iodine (Iodine-131 ama Iodine-123).
•Vipimo vya kuangalia kama figo zimeshindwa kufanya kazi vizuri kama;
a)Kipimo
cha utendaji kazi wa figo (Renal function tests) ambacho husaidia
kuchunguza kiwango cha urea (blood urea nitrogen (BUN) katika damu.
Aidha husaidia pia kuchunguza ongezeko la kiwango cha creatinine katika
damu.
b)Uchunguzi wa kiwango cha madini mbalimbali katika damu (blood electrolytes)
c)Kupima kiasi cha mkojo kinachotolewa na mgonjwa katika masaa 24
d)Uchunguzi wa mkojo (Urine analysis): Rangi ya mkojo, kiasi cha electrolytes, uwepo wa usaha au damu au casts.
e)Ultrasound ya figo na kibofu cha mkojo
f)Renal biopsy.
Tiba ya Gynecomastia
Kama
nilivyosema hapo awali, tatizo hili kwa vijana waliokatika umri mdogo
au wa kubaleghe hupotea lenyewe taratibu ndani ya miezi 18. Kwa mzazi
unatakiwa usihofu, lakini kama litaonekana kwa mtoto zaidi ya miaka 17,
basi hapa mzazi unatakiwa kuchukua hatua za haraka ambazo ni kumuona
daktari ili aweze kukusaidia kwa ufasaha zaidi.
1.Tiba ya madawa
•Tiba
ya kutumia vichocheo (Testerone Replacement Therapy) – Kichocheo aina
ya testerone hutolewa kwa mgonjwa kwa njia ya mdomoni, kwenye dripu, au
kipachiko (patch forms). Hii hutolewa kwa wagonjwa ambao hawawezi
kutoa testerone kutoka kwenye korodani zao kutokana na kupata ajali,
ugonjwa au wale ambao hawana korodani kutokana na sababu mbalimbali.
•Dawa
aina ya Selective Estrogen Receptor Modulator (SERMs) kama Tamoxifen,
raloxifen, husaidia kupunguza ukubwa (volume) wa matiti lakini
haziondoi tishu zote kwa ujumla. Aina hii ya tiba hutumiwa kwa wale
wenye tatizo sugu la gynecomastia au wale wenye kupata maumivu makali
sana. Dawa hizi zina madhara na hivyo ni vizuri kutumia kwa maelekezo
ya daktari.
•Dawa
aina ya Aromatase Inhibitors kama anastrozole, hufanya kazi kwa kuzuia
kimengenyo aina ya aromatase na hivyo kuzuia utengenezwaji wa
kichocheo aina ya estrogen. Tafiti nyingi zilizofanywa zimeshindwa
kutoa majibu ya uhakika juu ya matumizi ya dawa hizi katika kutibu
tatizo hili la kukuwa kwa matiti kwa wanaume.
2.Tiba
ya Upasuaji – Kwa wale wenye tatizo hili sugu, upasuaji wa kurekebisha
matiti unaweza kufanyika. Hii humuongezea mwanamume hali ya kujiamini
na hivyo kuwa katika hali nzuri kisaikolojia, na huongeza ufanisi wa
maisha yake ya kila siku.
3.Kupunguza uzito kwa kufanya mazoezi mara kwa mara na kula mlo wenye virutubisho vyote muhimu.
4.Kutibu chanzo au magonjwa mbalimbali kama hyperthyroidism, ugonjwa wa figo kushindwa kufanya kazi, saratani mbalimbali na nk.
5.Kuacha kunywa pombe na matumizi ya madawa ya kulevya kama bangi/marijuana.
6.Daktari
kumbadilishia mgonjwa dawa baada ya kuona dalili za tatizo hili kwa
wale wenye kutumia dawa za kutibu ugonjwa wa Ini, dawa za kurefusha
maisha. Kwa wagonjwa wa Ukimwi, ni vizuri kwa daktari kabla ya kumpa
mgonjwa dawa, kumfanyia mgonjwa kipimo cha fasting lipid profile, ili
uweze kutambua kama dawa unazotaka kumpa zitamletea madhara au la. Na
inashauriwa kurudia kipimo hiki kati ya miezi 3 hadi 6 baada ya kuanza
dawa hizi za kurefusha maisha au baada ya kumbadilishia mgonjwa dawa.
Hata hivyo sio dawa zote za kurefusha maisha zilizo na madhara haya,
kwani zipo nyingine zinazopunguza kiwango cha mafuta mwilini na kwenye
tishu.
Madhara ya Gynecomastia
1.Uwepo
wa tatizo hili kwa muda wa zaidi ya miezi 12 au mwaka mmoja,
husababisha matiti kutengeneza makovu au kwa kitaalamu
scarring/fibrosis na hivyo kufanya tiba kwa kutumia dawa kuwa ngumu
sana.
2.Wanaume
wenye tatizo hili wapo kwenye hatari zaidi ya mara tano ya kupata
saratani ya matiti ikilinganishwa na wanaume ambao hawana tatizo hili.
3.Kuathirika
kisaikolojia (kuona aibu, kutojiamini, kujihisi tofauti na wanaume
wenzake). Hali hii inaweza hata kumfanya mtu kuishi maisha ya huzuni
au kushindwa kujumuika na watu katika shughuli mbalimbali kama michezo
na nk
No comments:
Post a Comment