Wednesday 26 March 2014

Tahadhari kuhusu ugonjwa wa dengue nchini

Kutoka GAZETI LA MWANANCHI
Dar es Salaam. Wananchi wameaswa kuchukua hadhari juu ya ugonjwa wa dengue ambao dalili zake ziko sawa na zile za malaria. 
Mpaka sasa ugonjwa huo hauna tiba maalumu wala chanjo na njia pekee ya kukabiliana nao ni kutambua dalili zake kama vile homa, kupungukiwa maji au damu, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu. Mgonjwa anaweza kupoteza maisha endapo atachelewa kupatiwa matibabu.
Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Idara ya Habari wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja alithibitisha kuwapo kwa ugonjwa huo nchini tangu Februari,1914.
“Watu wengi wanaougua homa ya Dengue hukimbilia kumeza dawa za malaria jambo ambalo ni hatari kwa kuwa wanazidi kuchelewa kupata tiba inayostahili. Ni vyema mgonjwa aende hospitali kufanya vipimo vinavyostahili kutoka kwa wataalamu,” alisema Mwamwaja na kuongeza kuwa:
“Mtu mmoja amefariki na wengine 70 wamegundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo. Madaktari wetu wanajua kuwapo kwa ugonjwa huo na wamejizatiti kukabiliana nao,” alisema na kuongeza:
“Homa ya Dengue ni ugonjwa unaoenezwa na mbu aina ya Aedes na dalili hizi huanza kujitokeza kati ya siku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa. Ugonjwa hauenezwi kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine isipokuwa kupitia mbu huyo,”.
Kwa mara ya kwanza ugonjwa huo uligundulika Dar es Salaam mwaka 2010, ambapo jumla ya wagonjwa 40 walithibitika kuambukizwa. Idadi ya waathirika iliongezeka na kufikia 172 kati ya Mei na Julai mwaka jana, ila hakuna aliyepoteza maisha.
Licha ya kutoa taarifa kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya, Serikali inaendelea kuimarisha udhibiti wa ugonjwa huo kwa kuongeza umakini katika ufuatiliaji kupitia kwa wataalamu wake wa afya kote nchini. Hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa na Serikali kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini na Wizara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huo.
Nsachris alisema, hospitali zote za Serikali, wilaya na mikoa zinaweza kuwahudumia wagonjwa wa dengue kwa vipimo na matibabu.
Nchini India ugonjwa huo huathiri mamia ya wananchi wake , hasa wakati wa majira ya mvua ambao huambatana na homa kali, maumivu makali ya kichwa,  kuharisha na kutapika.

No comments:

Post a Comment

.