Chakula bora (Balanced diet) ni chakula kinachokupa virutubisho vyote muhimu mwilini katika milo mitatu ya siku. Chakula bora, kama ilivyo kwa kila kitu bora, hakiliwi kwa bahati, bali huhitaji mipango madhubuti ya kupanga chakula cha kila siku kinachojali afya yako na familia.
Sasa, kuandaa ratiba ya chakula kizuri si kazi rahisi, lakini inasaidia kupunguza mawazo ya nini cha kupika na kupunguza haraka za kuandaa vyakula bila kufikiria vizuri virutubisho vinavyopatikana kwenye milo yako. Kwa kawaida ni kazi ya mama kuamua chakula gani kinaliwa nyumbani. Lakini, mie nadhani ni swala la familia nzima kuamua chakula gani kinafaa kuliwa sababu chakula ni swala la kila mtu kwenye familia. Hapa ndio panapotuleta kwenye swala zima la kupanga ratiba ya chakula kwa wiki nzima. Chakula ni kitu muhimu sana maishani, hivyo ni jukumu la kila mtu kuchangia mawazo kwenye afya ya familia, si jukumu la kumuachia mama pekee - kila mtu ana nafasi yake kwenye kutoa mchango, hata kama ni wa mawazo.
Kama uko peke yako usikate tamaa, ni rahisi zaidi maana utakuwa una uwezo wa kufanya maamuzi bila kuwa na mawazo ya kukinzana.
Swala la kuamua chakula gani kinaliwa lini ni swala la mipango na malengo. Ukifanya hivi unaweza kujijengea ratiba ya kula milo vizuri iliyojaa virutubisho unavyohitaji. Na jambo kubwa hapa ni kuokoa muda na matumizi yasiyo na tija.
Faida za ratiba ya chakula
Je ni faida gani unapata kwa kupanga ratiba ya chakula?- Kufahamu kirahisi vyakula vyenye afya na kwa mahitaji yako. Mfano mzuri ni kuwa na uwezo wa kula matunda na vyakula vya protini kwa wingi
- Ni rahisi kujua virutubisho muhimu unavyokula kwa kipindi cha wiki nzima, hivyo ni rahisi kukusaidia kutathmini afya yako kwa urahisi
- Kuwa na chaguo zaidi ya moja ya vyakula hivyo kuzuia kula chakula aina moja kinachopendelewa na kusababisha kukosa virutubisho muhimu kwenye vyakula vingine
- Kupanga matumizi madhubuti ya nyumbani na kuweza kuokoa fedha kwenye maswala ya chakula. Usidharau sana hii sababu chakula ndio kitu pekee kinachotumia hela nyingi kupita kiasi kwa matumizi nyumbani. Ukiweza kujua vizuri matumizi ya nyumbani utakuwa na uwezo wa kupanga matumizi yako vizuri na kufanya shughuli za maendeleo.
- Ni njia pekee ya kuweza kujua afya yako halisi na familia yako – mfano kupunguza au kuongeza uzito
- Ni njia mbadala ya kuwafundisha watoto wako jinsi ya kuishi vizuri na vyema wakiwa watu wazima wenye familia zao. Watoto huangalia matendo yako, siyo maneno, hivyo ni vizuri kuwaanzishia msingi mzuri wa maisha ili wapate kufaidika na maisha yako hapo baadae.
- Kudumisha furaha nyumbani sababu kila mmoja anaona umuhimu wake katika mawazo juu ya chakula, hivyo kuwafanya watu kufurahia kujumuika kula pamoja kifamilia.
Jinsi ya kupanga ratiba ya chakula
Je unawezaje kuweka uwiano bora wa vyakula ili uweze kupata virutubisho muhimu mwilini ?Ni vizuri kuwa na ratiba ya chakula kwa wiki nzima, hii itasaidia kujua milo ya chakula kila siku na jumla ya virutubisho unavyopata mwilini. Ratiba ya wiki inasaidia kujua ni kiasi gani cha chakula kinahitajika kwako (kama uko peke yako) au familia kwa ujumla.
Unaweza kupanga ratiba yako kama unavyopenda. Ila ni muhimu kufuata maagizo machache yafuatayo :
1. Hakikisha unapata vyakula muhimu
Angalia aina muhimu za vyakula kwa siku –
matunda na mboga za majani. Hizi ni muhimu kuwepo sababu zina
virutubisho halisi vinavyohitajika mwilini. Ni vizuri kula matunda na
mboga za majani zisizopungua aina 5 kwa siku. Mfano wa matunda ni ndizi,
papai, nanasi, apple, chungwa n.k.
2. Kuwa mbunifu
Kula ni haki yako, lakini kwanini ule
chakula aina moja wakati kuna vyakula vingi tu vitamu? Jifunze kuandaa
vyakula tofauti, kula kwa rafiki, onja vyakula aina mbalimbali. Ili
kuweza kutimiza hili, jaribu kula vyakula tofauti kutokana na ratiba
yako. Ni muhimu kutopendelea vyakula kwenye kundi moja sababu unakosa
virutubisho kutoka kwenye kundi tofauti.
Kama kuna kitu unapendelea zaidi, weka
kiwe kinapatikana mara nyingi kwenye ratiba yako. Lakini jaribu na
kwengine uone ubora wake. Mfano mzuri ni kuwa mie hupendelea zaidi
maharage, ni jambo zuri kula chakula nikiwa na maharage pembeni.
3. Pendelea vitu halisi
Ni rahisi sana kula vyakula visivyo na
virutubisho nyumbani sababu ndio vyakula vilivyojaa kila kona ya dunia
kwa sasa. Ili kuhakikisha unakuwa na afya bora, pendelea zaidi vitu
halisi kuliko vile vya kuchakachua – kunywa maji badala ya juisi. Kula
tunda badala ya juisi. Maji ni muhimu sana, lakini wengi tunapuuzia hii
kanuni ya afya. Mfano, mtu mzima anatakiwa kunywa lita moja na nusu ya
maji kwa siku. Je unazingatia hilo ?
Tunashauri uwe na ratiba ya chakula nyumbani. Ni vizuri kwa afya pia
kwa kujua vizuri matumizi ya nyumbani. Mie huwa nafanya hivi kila
wakati, nimeona faida zake ndio maana nakushauri na wewe. Kama umependa
basi washauri na wenzio, maana kila kitu kizuri ni vyema kuwaeleza wale
tuwapendao.KUTOKA MISOSI.COM
No comments:
Post a Comment