Maafisa wa serikali kuu ya Marekani pamoja na wale wa jimbo la Texas
wamewawekea karantini watu wanne wa familia ya mtu aliyegunduliwa kuwa
na ugonjwa wa Ebola huku maafisa wa Liberia wakisema watamfungulia
mashtaka mtu huyo kwa kudanganya kwenye hati za kusafiria katika uwanja
wa ndege wa Liberia.
Mgonjwa huyo anayetambuliwa kwa jina la Thomas Duncan raia wa
Liberia ni mgonjwa sana lakini anajitambua na ametengwa katika hospitali
moja ya Dallas nchini Marekani.
Maafisa wa Liberia wanasema watamfungulia mashtaka Duncan ambaye
alipanda ndege kutoka Liberia na kuwasili huko Texas Septemba 20, kwa
shutuma za kudanganya kwenye hati za uwanja wa ndege wa Liberia wakati
alipoulizwa kama alikuwa na mawasiliano na mtu yeyote aliyekuwa
anaugua maradhi ya Ebola.
Duncan anaripotiwa kujibu ‘hapana’ kwenye swali hilo japokuwa
alimsaidia mwanamke mmoja mjamzito aliyekuwa anaugua ugonjwa wa Ebola
kuingia katika taxi.
Wakati huo huo nchini Liberia mpiga picha wa Marekani anayefanya kazi
na kituo cha televisheni cha NBC News ameambukizwa Ebola. Taarifa
zinasema mtu huyo anasafirishwa kurudi Marekani na wafanyakazi wote
wanaomsaidia watakua kwenye karantini kwa siku 21.
Shirika la afya duniani-WHO linaripoti kwamba zaidi ya watu 3,000
wamekufa na Zaidi ya 7,000 wameambukizwa ugonjwa huo katika nchi za
Guinea, Liberia na Sierra Leone
No comments:
Post a Comment