Friday 10 October 2014

CHUKUA HATUA KUHUSU UGONJWA WA SURUA KWA KUEPUKA ATHARI HIZI.

Surua ni mojawapo ya magonjwa ya kuambukiza yanayotisha kwa binadamu. Huu ni ugonjwa ulio na kiwango cha juu cha karibu asilimia 100 cha mashambulizi pindi mtu apatapo vimelea vya ugonjwa huu.
Surua huzuiwa kwa urahisi kwa njia ya chanjo. Watoto ambao hawajapata chanjo ya surua wapo katika hatari kubwa sana ya kupata surua

Pamoja na kuwepo chanjo ya ugonjwa huu, bado surua ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo vingi vya watoto walio chini ya umri wa miaka 5 katika baadhi ya maeneo duniani hasa kwa nchi zinazoendelea. Ugonjwa huu ambao ulitoweka katika baadhi ya nchi, umeanza kuonekana tena hivi karibuni miongoni mwa watu ambao hawakupata chanjo katika nchi za Uingereza na nyingine za Ulaya.
Athari za Surua ni zipi?
Ingawa baadhi ya wagonjwa hupona katika kipindi cha siku 10 mpaka 14, baadhi hupata matatizo zaidi yanayoweza kuwa ya muda mrefu kama;
  • Maambukizi njia ya masikio (Otitis media)
  • Maambukizi njia ya chini ya mfumo wa hewa kama vile
    • Uambukizi kwenye mirija ya hewa ya koo (bronchitis) maambukizi kwenye njia ya sauti (laryngitis) na croup. Surua inaweza kusababisha kuvimba katika sehemu ya sauti na kuathiri uwezo wa kutoa sauti lakini vilevile inaweza kusababisha uvimbe katika kuta za utando wa njia ya hewa.
    • Homa ya mapafu (pneumonia) ambayo ni sababu kuu inayosababisha vifo vinavyotokana na surua. Mgonjwa wa surua ni rahisi kupata homa ya mapafu kwa sababu kinga ya mwili wake huwa imepungua. Homa hii ya mapafu yaweza kusababishwa na aina nyingine ya virusi kama adenovirus, herpes simplex au bakteria kama Staphylococcus aureus, Streptococcus pneumonia, Haemophillus influenza, Klebsiella pneumonia. Lakini vilevile Kifua kikuu kinaweza kutokea kwa kusababishwa na upungufu huu wa kinga mwilini.
  • Surua pia inahusishwa na aina mbalimbali ya mashambulizi kwenye ubongo kama vile
    • Acute encephalitis ambayo hutokea wakati au ndani ya wiki chache baada ya maambukizi.
    • Progressive encephalitis ambayo hutokea kwa wagonjwa walio na upungufu wa kinga mwilini unaotokana na sababu yeyote ile ikiwemo wale anaopata tiba ya kemikali (Chemotherapy) au kwa sababu ya VVU. Hali hii hutokea miezi 6 baada ya maambukizi, na inaweza kusababisha mgonjwa kufa.
    • Subacute sclerosing panencephalitis (SSPE) ni nadra sana kutokea. Iwapo ikitokea, mara nyingi huwa ni mwaka mmoja wa mgonjwa kupona surua. Dalili mojawapo ya tatizo hili ni kupungukiwa kwa uwezo wa kufikiri, akili kuzorota na hatimaye mgonjwa kufariki dunia.
  • Surua inaweza kusababisha utapiamlo kwa sababu ya ukali wake hasa kwa watoto ambao hawapati lishe nzuri. Inahusishwa pia na kuharisha na kutapika na kusababisha upungufu wa maji mwilini.
  • Surua husababisha upungufu wa Vitamini A na kusababisha tatizo la kutoona vizuri ambalo hijulikana pia kama Keratitis. Kwa mtoto ambaye ana upungufu wa Vitamini A tatizo la macho huwa kubwa zaidi na kwa kitaalamu hujulikana kama Keratomalaciaambapo sehemu nyeupe ya jicho hutoboka.
  • Maambukizi katika misuli ya moyo (Myocarditis)
  • Upungufu wa chembe sahani kwenye damu (Thrombocytopenia)

No comments:

Post a Comment

.