Katika njia muhimu alizopendekeza ni pamoja na hizi hapa:
1. Kubadilisha vyombo vya chakula vya mtoto
Mtoto huvutiwa zaidi na rangi, hasa kwenye vitu anavyotaka kula. Mtoto anaweza kuchoka kula chakula sababu anatumia chombo kimoja kila siku, hii haijalishi kama chakula kinabadilika au la. Ni muhimu kumuandalia mtoto chakula kwenye vyombo vyenye rangi na maumbo tofauti. Na ushauri wa daktari ni kuwa, usirudie chombo kwa wiki nzima, kama inawezekana. Hii inamfanya mtoto kuona utofauti wakati wa kula, na kumfanya apate hamu ya kula.Mfano, unaweza kutumia bakuli, vikombe, sahani, vijiko vyenye rangi tofauti ili kumfanya aone anakula katika mazingira tofauti na hii humfanya awe na hamu kula chakula zaidi.
2. Watoto wale pamoja na familia
Watoto hupenda kuiga wazazi. Mara nyingi sana watoto hupewa vyakula wale wakiwa wenyewe wakati watu wengine wanaendelea na shughuli za kawaida. Hii inaweza kumfanya mtoto kupendelea zaidi kucheza kuliko kula. Ni muhimu kumlisha mtoto wakati familia nzima imekaa mezani au jamvini tayari kwa kula. Katika muda huu mtoto atakula vizuri bila vikwazo, maana kila mmoja anakula.
Vilevile, watoto wengine (umri wa miezi 10 hadi miaka 2) hupendelea kula vyakula wanavyokula watu wazima, hata kama haviwafai, na kugoma vyakula vya watoto. Ni bora kumuandalia chakula kinachofanana na unachokula wewe na kumpa ili apate kufurahia. Huwezi kubishana na mtoto, ingawa huwezi kumpa kila kitu anachotaka pia. Ila jaribu kutumia mbinu tofauti ili apate kula na kuridhika. Afya yake ni bora kuliko kitu kingine kwenye maisha yake kwa muda huu.
3. Jaribu kumsoma mtoto anapenda nini
Kila mzazi ana jukumu la kumsoma mwanae anapendelea nini. Ili kuweza kumfanya mtoto ale vizuri, ni vyema kubadilisha vyakula kila wakati – siyo kila siku. Mara nyingi watoto huchukua muda kuzoea chakula, hivyo ni vizuri kumpa mtoto chakula kwa muda wa siku 2 hadi 3 na kumbadilishia na chakula kingine. Hii inasaidia mtoto kuonja ladha ya chakula. Anaweza kukipenda au kukichukia. Kama atakataa ladha ya chakula kipya, usikate tamaa, jaribu kumpa tena baada ya siku moja au mbili, unaweza kukuta akaipenda ladha na akala chakula bila tatizo.
Usikate tamaa kwenye kumpa mwanao upendo wako kama mzazi. Jaribu kila njia unayoweza na usife moyo. Watoto ni wagumu kuwaelewa na inachukua muda, lakini pale unapofikia hatua ya kujua anachopenda utakuwa umepata jibu zuri jinsi ya kuendelea kumlea mwanao.
4. Epuka kumpa vitu vitamu kati ya milo
Watoto wengi wanapenda kula vitu vidogo vidogo (pipi, biskuti, juisi, keki n.k.) kila mara. Hivi vitafunwa vinaweza kumfanya mtoto azibe njaa na kutokuwa na hamu ya kula chakula muda unapowadia. Ili kuzuia hii tabia, ni bora kuacha kumpa mtoto vitu vidogo vidogo kati ya milo ili kumfanya kuwa na hamu ya chakula muda unapowadia.
Mara nyingi inashauriwa kumlisha mtoto mara 4 hadi 5 kwa siku. Hii ni vizuri sababu mwili wa mtoto unakuwa unahitaji virutubisho vingi mara kwa mara kwa kusaidia kukua. Ni vizuri kumpa mtoto chakula bora kuliko kumjaza tumbo na vyakula vyenye sukazi zisizo na kazi mwilini.
5. Msikilize mtoto anachotaka
Mara nyingi mzazi au mlezi unaweza kudhani kuwa unajua zaidi kiwango cha chakula anachotakiwa kula mtoto kuliko hata mtoto mwenyewe. Hili linaweza kuwa tatizo kubwa litakalopelekea mzazi kumlazimisha mtoto kula chakula kingi kupita kiasi. Fahamu kuwa, watoto wanajua kiwango cha chakula kinachowatosha na wakati gani ni muafaka wa kula. Hivyo, itakuwa rahisi kwako kama ukimsikiliza mtoto anataka nini, kuliko kulazimisha kile unachotaka wewe. Hakuna mtoto anayeweza kuvumilia kukaa na njaa. Watoto wote huhitaji chakula ili kucheza na kufurahi na wenzao. Hivyo basi, pale anakuwa na njaa atasema, au kulia, na ndio muda muafaka wa kumpa chakula unachotaka.
Swala muhimu la kuzingatia ni kuwa, katika mazingira yeyote, usimlazimishe mtoto kula. Usimkabe. Kulazimisha mtoto kula ni kumjengea tabia ya kuchukia chakula. Na akishajenga tabia hii hawezi kuacha sababu atakuwa anahusisha chakula na adhabu. Hakuna mtu anayependa adhabu. Hivyo, watu wengi wanaopenda kulazimisha mtoto kula kwa kumkaba huwa wanajenga tatizo kubwa zaidi ya lile la kula tu.
No comments:
Post a Comment