Kutokana
na asili katika uumbaji pamoja na ambavyo sisi wanadamu tumezoea kuona,
ni kwamba ni jambo la kawaida kwa mwanamme kuota ndevu.
Lakini
endapo ndevu zitaonekana zimeota kwa mwanamke, basi kwa baadhi ya watu
wataanza kujiuliza ni kwa nini na pengine wakawa na mitazamo tofauti juu
ya mwanamke huyu ambaye ameota ndevu. Baadhi watamuona mwanamke huyu
kuwa ni mchafu na asiyejipenda na mitazamo mingine mingine ya tofauti.
Kuna mambo mengi ambayo huweza
kumfanya mwanamke aote ndevu, na pengine baada ya kukufahamisha utaweza
kupata mtazamo wa tofauti juu ya hali hiyo ya kiafya inayojitokeza kwa
mwanamke.
Katika
mfumo mzima wa uzazi, ndani ya mwili wa mwanamke, kuna viungo
vinavyohusika na utoaji wa mayai ambayo baadae huja kurutubishwa na
mbegu za kiume na kupelekea mwanamke kupata ujauzito. Viungo hivi
vinavyotoa mayai ambavyo huitwa kitaalamu Ovaries, katika hali ambayo
siyo ya kawaida Ovaries hizi huzungukwa na kitu kama ngozi na hivyo
kupelekea zishindwe kutoa mayai, tatizo ambalo kitaalamu hujulikana
kama, Polycystic Ovarian Syndrome (PCOS). Baada ya mayai hayo kushindwa
kutoka, hupelekea mwanamke kushindwa kuona siku zake, hedhi, au
kuvurugika kwa tarehe ambazo alikuwa amezoea kupata hedhi.
Pamoja
na mwanamke kushindwa kupata hedhi, pia miongoni mwa dalili
zinazoambatana na tatizo la kufunikwa kwa Ovaries,PCOS, ni kuongezeka
kwa homoni za kiume (Androgens) katika mwili huu wa mwanamke.
Ikiwa ni
pamoja na kazi nyingine zinazofanywa na homoni hizi za kiume,
androgens, pia homoni hizi huhusika na uotaji au ukuaji wa nywele
mwilini, na miongoni mwa sehemu ambazo homini hizi hufanya kazi kiharaka
ni kama vile maeneo ya kifuani, kidevu, midomo ya juu (Upper lips)
pamoja na kwenye mapaja.
Hivyo
tatizo hili, PCOS, kwa kuwa huambatana na kuongezeka kwa homoni za kiume
mwilini, basi humsababisha mwanamke aote ndevu au nywele katika maeneo
hayo niliyoyataja hapo juu. LAKINI, napenda uelewe kuwa tatizo hili la
PCOS humsababisha mwanamke aote ndevu, ila SIYO kila mwanamke aliyeota
ndevu analo tatizo la PCOS, inawezekana akawa na ongezeko la homoni za
kiume lililosababishwa na mambo mengine kama vile matumizi ya dawa.
Kwa mwanamke mwenye tatizo hili la kuota ndevu, kwanza aonane
na daktari wake au wataalamu wa afya ili waweze kugundua chanzo cha
tatizo hilo ili waweze kuandaa mfumo mzuri wa kumsaidia, na pia kama
wanajamii tusiwatenge na kuwaona wanawake hawa kuwa ni wa ajabu katika
jamii, bali tuwape ushirikiano na kuwapa msaada unaostahili ili waweze
kutatua tatizo au hali hiyo ya kiafya kwao.
No comments:
Post a Comment