Kifua kikuu (TB), ugonjwa
huu husababishwa na bakteria waitwao Mycobactrium tuberculosis. Bacteria
hawa (chembechembe za ugonjwa) hushambulia mapafu ya hewa. Ukikaa karibu
na mgonjwa mwenye T.B. waweza kuambukizwa ugonjwa huo kwani akikohowa hutoa
vijidudu hivyo vikasambaa hewani.
Kifua kikuu cha mapafu ni
ugonjwa unaoambukiza kwa urahisi sana. Walio na hatari zaidi ya kuambukizwa
ugonjwa huu ni wale ambao ni dhaifu, wakosefu wa lishe bora na wale wanaoishi
na mtu mwenye ugonjwa huo.
Ili kukijinga na kumponyesha
mgonjwa aliyekwisha upata ugonjwa huo ni lazima mgonjwa atibiwe mapema.
Na hili haliwezekani mpaka dalili zake zifahamike.
Dalili za kawaida:
Kikohozi cha muda mrefu hasa
mara tu baada ya kuamka; homa ndogo ndogo nyakati za mchana na kutoka jasho
jingi wakati wa usiku. Kuwa na maumivu kifuani au sehemu za juu ya mgongo.
Kukonda na kuwa dhaifu muda mrefu (daima) ni dalili nyingine muhimu.
Mtu akifikia hatua ya kuzidiwa
dalili zifuatazo zitajitokeza. Kukohoa damu, ngozi kuwa laini na inayofifia
pamoja na sauti kukwaruza. Dalili hii ya sauti kukwaruza ni mbaya sana.
Ilivyo kawaida kifua kikuu
ni ugonjwa wa mapafu lakini kinaweza kutokea sehemu yoyote ya mwili ikiwemo
mifupa na utumbo.. Kwa watoto wadogo kinaweza kusababisha homa ya uti wa
mgongo.
Ipo pia TB ya ngozi au tezi
na husababishwa na vijidudu vile vile vinavyosababisha kifua kikuu.
Kwa kawaida TB ya ngozi hukua
taratibu na hudumu muda mrefu. Pia huambukiza tezi hasa zile za shingo
au sehemu zile za mtulinga kati ya bega na shingo. Tezi zinazovimba hupasuka
na kutoa usaha, kisha hufunga kwa muda na kupasuka tena ila kwa kawaida
haziumi.
TB hii husababisha uvimbe
unaoharibu uso, mabaka ya vidonda yasiyotoweka, donda ndugu au chunjua
kubwa.
TB ya ngozi hutibiwa kama
ile ya kifua kikuu. Ili kukomesha isirudie tena ni lazima kutumia dawa
kwa muda mrefu (miezi mingi) baada yakuona hali ya ngozi imekuwa nzuri.
Mtu akihisi dalili za kifua
kikuu ni lazima amuone mganga haraka ili afanyiwe uchunguzi wa ngozi, makohozi
na kupiga picha (X-Ray) ya kifua.
Dawa mashuhuri kwa kutibu
ugonjwa huu ni sindano ya 'Streptomisini', vidonge vya 'Para-aminosalicylici
acid (P.A.S.),vidonge vya isoniacid, vidonge vya Ethambutal
na Thiazetazone. Dawa hizi mara nyingi huchanganywa za aina mbili
au tatu.
Kwa kawaida huchukua muda
wa mwaka mmoja na zaidi hadi kupona kabisa. Hivyo ni lazima mgonjwa aendelee
kutumia dawa hata kama ataona hali yake imekuwa nzuri.
Mambo yakuzingatia:
Kula chakula kingi chenye wingi wa protini, vitamini na cha kukupa nguvu.
Lazima kupumzika.
Acha kabisa kufanya kazi. Pumzika na lala usingizi wa kutosha.
Nyumba ikishakuwa na mgonjwa
wa kifua kikuu yafuatayo yafanyike: Mgonjwa ale na kulala peke yake, ikiwezekana
chumba cha peke yake. Watoto wawe mbali naye na wapewe dawa ya kinga (Vaccination).
Mgonjwa anapokohoa ahakikishe kuwa anafunika kinywa chake. Mgonjwa atibiwe
mara moja. Familia izidishe kula chakula bora na ifanyiwe uchunguzi wa
ugonjwa huu.
Kwa mtu aliye na virusi vya
ukimwi (Human Immunodeficiency Virus- HIV) yupo katika hatari zaidi ya
kupata TB kwa sababu virusi vya HIV hudhoofisha nguvu na uwezo mwili kujikinga
na magonjwa.
--
No comments:
Post a Comment