Geita. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Geita, Magreth Nakainga amemvua madaraka Mganga Mkuu wa
Zahanati ya Nyakabale, Josephat Msafiri kwa kukiuka miiko ya kazi yake
na kulewa wakati wa kazi.
Mkurugenzi huyo aliamua kuchukua uamuzi huo jana
kutokana na tukio lililotokea Juzi hii la daktari huyo kufunga kituo cha
afya na kuacha wagonjwa wakiwa wamezidiwa, kisha kwenda kunywa pombe
jambo lililowalazima kumchapa viboko akiwa baa.
“Tumeshamchukulia hatua za kinidhamu ikiwa ni
pamoja na kumvua madaraka yake ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wa
Serikali,” alisema Nakainga.
Alisema kitendo alichokifanya kimeidhalilisha taaluma ya afya na madaktari kwa ujumla.
Alisema tabia kama hizo hazitavumilika kwa mtumishi yeyote atakayekiuka maadili ya kazi.
Pia alisema amepeleka wahudumu wa afya wakiwamo
wauguzi wawili na daktari mmoja katika zahanati hiyo na huduma
zinaendelea vizuri.
Alipopigiwa simu jana ili azungumzie uamuzi huo,
daktari huyo alianza kumlaumu mwandishi aliyeandika habari ya tukio hilo
akisema kuwa amemharibia kazi.
“Sikutegemea kama wewe uko hivyo, sasa nimekujua
kumbe uko hivyo, Mungu mkubwa, yaani mmepigiwa simu na watu na kuamua
kuja kuniharibia,” alisema Dk Msafiri na kukata simu kisha akaandika
ujumbe uliosema: “Sikukujua sasa nimekujua vizuri, Mungu mkubwa.
No comments:
Post a Comment