Thursday 25 December 2014

MADHARA NA TIBA YA MAPUNYE

Katika makala yetu Leo hii tunaangalia maradhi ya fangasi yanayoshambulia kichwa au mapunye ambayo kitaalam huitwa Tinea capitis.
Mapunye  au Tinea Capitis ni nini?
Aina hii ya maradhi ya fangasi hushambulia eneo la kichwa pekee ukiacha eneo la uso. Kwa maneno mengine, aina hii ya fangasi haishambulii uso bali hushambulia eneo lililobaki la kichwa.
Huwashambulia kina nani?
Haya hushambulia watu wote wa jinsia na umri wote, ingawa huonekana zaidi kwa watoto wadogo. Fangasi hawa hushambulia watoto wadogo ambao hawajafikia umri wa balehe na mara nyingi huacha kushambulia pale mtoto anapofikia umri huo wa balehe.
Mwonekano wake
Mapunye huweza kushambulia eneo lote la kichwa au sehemu tu ya kichwa. Eneo la ngozi ambalo lina mashambulizi ya mapunye huwa na umbo linalofanana na sarafu.
Eneo hili la ngozi lililoathirika kama lina nywele, basi hunyonyoka na hivyo mwonekano wa mfano wa sarafu huonekana vizuri tu hata bila kutumia jicho la kitaalam.
Dalili zake
Ukiachilia mbali mwonekano wa mapunye kama nilivyoeleza hapo juu kuna dalili nyingine za maradhi haya.  Hizo ni:
-Eneo la ngozi lililoshambuliwa kuwasha (ingawa si mara zote)
-Kubadilika kwa rangi ya ngozi ya eneo lenye maambukizi
-Ukitazama kwa makini eneo ambalo lina mashambulizi ya maradhi haya utagundua kuna vidoti vyeusi ambavyo vinaonyesha eneo ambalo nywele imeng`oka kutokana na maradhi.
-Ngozi kubanduka kwenye eneo lenye maambukizi
-Ngozi kukauka kwenye eneo lenye maambukizi
-Mara nyingine usaha pia huweza kuonekana kwenye eneo la ngozi lililoshambuliwa na fangasi hawa (hii kwa kitaalam huitwa kerions)
-Kama maradhi haya yakikaa bila kutibiwa kwa muda mrefu husababisha dalili nyingine kuonekana kama kutoka kwa maji maji kwenye eneo la ngozi lililoathirika pamoja na kutoka kwa harufu mbaya kwenye eneo la ngozi lililoathiriwa na vimelea hivi vya fangasi.
Yanavyosambaa
Kuna njia nyingi zinazoweza kusababisha uambukizi wa mapunye lakini ili uambukizaji huu uwezekane lazima kuwa na mazingira rafiki ya kuwezesha fangasi kuweza kuishi na kuhama kwa urahisi. Mazingira haya rafiki kwa kuruhusu fangasi hawa kuweza kutoka kwenye kichwa cha mtu mmoja kwenda kwa mwingine huhitaji uwepo wa hali ya joto pamoja na majimaji (unyevunyevu).
Huwa ni rahisi sana kwa mapunye kuambukizwa kutoka kwenye kichwa cha mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia hizi:
-Kutumia vifaa vya kunyolea kwa zaidi ya mtu mmoja bila kuvifanyia usafi wa kuua vimelea kama fangasi wa aina hii
-Kutumia taulo au nguo ya kujikaushia kwa mtu zaidi ya mmoja hasa pale ambapo mmoja wa watumiaji hao ana maambukizi ya fangasi.
-Kutumia vifaa vya nywele kama chanuo la kuchania nywele kwa zaidi ya mtu mmoja hususani pale ambapo mmoja wa watumiaji hao ana maambukizi ya vimelea vya fangasi hao.
-Kugusana na mtu aliye na maambukizi tayari
-Kushirikiana mavazi aina ya kofia na mtu aliyekwisha pata maambukizi hayo
Ni nani yuko hatarini?
Watu ambao huweza kupata maambukizi ya mapunye ni wafuatao:
-Wale wanaoshirikiana na wenzao vifaa vya kunyolea bila kuvisafisha vizuri
-Wanaoshirikiana vifaa vya kufanya usafi wa mwili zikiwamo taulo
-Wanaotoka jasho hasa kichwani kwani huweza kuweka mazingira mazuri zaidi kuruhusu maambukizi yatokee kirahisi
-Wanaofanya kazi zinazohusisha uwekaji vichwa kwenye maji yaliyotuama kwa muda mrefu
-Wale ambao tayari  wana fangasi za kichwani kwani ni rahisi kwa fangasi hao kujirudia.
-Wanaofanya usafi wa mwili kwa kutumia maji yaliyobeba vimelea
-Wasiojikausha vichwa baada ya kuoga au kufanya usafi wa kichwa
-Watu wenye maradhi yanayosababisha kushuka kwa kingaikiwamo  kisukari.
-Wale wanaokunywa dawa za kuua vimelea (antibayotiki) kwa muda mrefu
-Watoto wadogo ambao hawajafikia umri wa balehe.
Jinsi ya kuyatambua
Mara nyingi aina hii ya fangasi hugundulika kwa macho hasa kwenye maeneo ambayo  fangasi  hao wapo kwa wingi. Kwa kutazama ngozi ya sehemu ya kichwa iliyoathirika na maambukizi ya fangasi hao, utaweza kuona madhara yanayokukabili.
Kwenye uhitaji wa vipimo basi sehemu ya ngozi iliyoathirika huchukuliwa kwa ajili ya kufanya vipimo vya maabara na kuangalia aina sahihi ya fangasi.
Matibabu
Mara nyingi mapunye hutibika kwa  dawa za kutibu fangasi za kupaka ambazo hutibu mapunye na kuyaponyesha kabisa bila kuhitaji kutumia dawa za kumeza. Hii ni kwa kuwa ni rahisi kwa dawa ya kupaka kupenya kwenye ngozi na kusababisha matokeo yanayohitajika.
Matibabu ya mapunye huchukua muda mfupi kuonyesha matokeo mazuri au  
Matokeo chanya mara zote, ila pia huwa ni rahisi kwa maradhi hayo kurudi  baada ya kumaliza matibabu kama hatua madhubuti za kujikinga na maradhi haya hazitochukuliwa.
Kwa sababu hiyo,  ni vizuri kwa mgonjwa wa fangasi kutumia dawa mpaka wiki mbili baada ya dalili za maradhi kutoweka.
Pia, ni vizuri dawa zake ukashauriwa na daktari
Kulingana na jinsi ulivyoathirika na Mapunye hayo.
Jinsi ya kujikinga
Kuna mbinu mbalimbali za kujilinda usipatwe na fangasi:
-Hakikisha mwili wako hasa kichwani yanabaki na ukavu muda wote
-Osha nguo, taulo na mashuka kuhakikisha fangasi wanaondolewa
-Epuka kushirikiana vifaa vya kunyolea nywele hasa kama hakuna namna ya kuvisafisha na dawa maalum ya kuua vimelea kabla hujatumia
-Epuka kushirikiana katika utumiaji wa vifaa vya kufanya usafi wa mwili kama mataulo.  Kama kazi yako inahusisha ukaaji wa muda mrefu kwenye maji basi hakikisha unakausha  mwili hasa sehemu za kichwa au uweke dawa ya kuzuia fangasi kwenye maji hayo.

DAWA YA MAPUNYE KWENYE KICHWA FANYA HIVI:

Ndimu au limau: Kabla kwenda kukoga jisugue limau ndani ya kichwa na baadae yale maganda ya limau yatie katika maji ya kukoga yaani yawe maji ya Uvuguvugu halafu ukoshe kwa maji yale kwanza na baadae utumie maji yaliyo safi. 

(Fenugreek) kwa lugha ya kiswahili inaitwa Uwatu. Uwatu unachukua vijiko 2 vya chai vya Uwatu (fenugreek) unazirowesha katika maji usiku mzima ili zipate kulainika, halafu unazipoda ponda na baadae unapakaa ndani ya kichwa na uwache kwa muda wa saa moja na baadae kuzikosha ikiwa utafanya hivi siku zote mbaa wataondoka Inshallah bila tabu yoyote.

KUTOKA http://mzizi-mkavu.blogspot.com/2014/05/afya-kwa-ngozi-mapunye-na-athari-kwa.html

No comments:

Post a Comment

.