Dar es Salaam. Wakati Taifa likikabiliwa na changamoto kubwa ya
uhaba wa dawa hospitalini, aina mpya na hatari zaidi ya ugonjwa wa kifua
kikuu sugu imegundulika na kuathiri mtu mmoja nchini.
Mgonjwa huyo alibainika kuwa na kifua kikuu sugu
kisicho na tiba, aina ya ‘Xtreme Drug Resistant’ au XDR-TB ambayo hapo
awali haikuwa ikiwaathiri Watanzania.
Huyu ni mgonjwa wa pili kubainika kuwa na aina hii hatari ya TB baada ya kesi ya kwanza kuripotiwa mwaka 2011.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa
XDR-TB ni nadra sana ambapo ni nchi 77 tu duniani ikiwamo Tanzania
zimeripoti tatizo moja moja, mwishoni mwa mwaka 2011.
Taarifa zilizokusanywa na WHO kutoka katika mataifa mbalimbali duniani zinahakiki kuwa kuna asilimia tisa tu ya kesi za XDR-TB.
MDR-TB ni kifua kikuu sugu ambacho kimeshindikana kutibika kwa dawa za mstari wa pili.
Mratibu wa Ugonjwa wa Kifua Kikuu Mkoa wa
Kinondoni, Dk Hassan Lupinda alithibitisha kupokewa kwa mgonjwa huyo na
kusema kuwa alipokelewa katika Hospitali ya Mwananyamala na vipimo
pamoja na historia yake ilibainisha kuwa ana TB aina ya XDR.
“Ni kweli tumempokea mgonjwa huyo ambaye ni
Mtanzania aliyekuwa akitokea Afrika Kusini, na sasa tayari tumempeleka
Kibong’oto wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kwa matibabu,” alisema.
Wakati huohuo, takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii zinaonyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa kifua
kikuu ambapo idadi ya watu waliopimwa mwaka 2013 imeongezeka kutoka 11,
640 mwaka 2009 hadi 20,469,241 mwaka 2013.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace
Maghembe alisema kwa kawaida mgonjwa wa aina hiyo anapopokelewa
hupelekwa Kibong’oto kwa matibabu zaidi.
Dk Maghembe alisema kwa sasa wagonjwa wengi
wanapelekwa karantini ya Kibong’oto wakati matengenezo ya karantini ya
Sinza yakiendelea.
“Tutakapokamilisha karantini hii ya Sinza tutakuwa na uwezo wa kuwahifadhi baadhi ya wagonjwa wa TB sugu hapa jijini,” alisema.
KUTOKA http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/TB-hatari-yaingia-nchini/-/1597296/2571032/-/10wam8o/-/index.html
KUTOKA http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/TB-hatari-yaingia-nchini/-/1597296/2571032/-/10wam8o/-/index.html
No comments:
Post a Comment