Kwa takribani miongo mitatu sasa, tumeshuhudia ongezeko
kubwa la mlipuko wa ugonjwa wa mkanda wa jeshi linaloendana na ongezeko
la hususani ugonjwa wa UKIMWI. Hali hii imefanya baadhi ya watu kuamini
kuwa, ugonjwa huu ni dalili ya wazi kabisa ya mtu kuwa na VVU, imani
ambayo kwa kiasi kikubwa ina ukweli ndani yake ingawa si kwa wote wanaopatwa nao.Mkanda wa jeshi au shingles au herpes zoster kwa majina ya
kitabibu ni ugonjwa unaosababishwa na virus wa aina ya Varicella-zoster
ambao pia husababisha ugonjwa wa tetekuwanga au chickenpox. Ugonjwa huu
huathiri ngozi ambapo huambatana na vipele na michubuko kama ya
kuungua yenye kuambatana na maumivu makali .
Visababishi
Kama tulivyokwisha tangulia kueleza hapo juu,
ugonjwa huu husababishwa na virus aina ya Varicella-zoster ambao pia
husababisha ugonjwa wa tetekuwanga. Baada ya mtu kupatwa na tetekuwanga,
virus hawa hubaki katika hali ya kupooza/kutokuwa na madhara (dormant)
katika neva fulani za mwili. Baada ya miaka kadhaa, iwapo itatokea
kinga ya mwili ikashuka kwa sababu yoyote ile, virus hawa hupata tena
nguvu/kuwa na madhara (active), kuibuka na kusababisha ugonjwa wa mkanda
wa jeshi.Kwa kawaida shambulio la mkanda wa jeshi hutokea mara moja maishani ingawa laweza kujirudia.
Vihatarishi
Mkanda wa jeshi unaweza kumpata mtu wa umri wowote ule ingawa watu walio katika makundi haya wapo katika hatari kubwa zaidi:
• Wenye umri wa zaidi ya miaka 60
• Mtu aliyewahi kuugua ugonjwa wa tetekuwanga kabla ya umri wa mwaka mmoja
• Watu ambao kinga yao ya mwili imepungua kwa
sababu mbalimbali kama vile matumizi ya aina fulan za dawa, magonjwa
kama vile maambukizi ya VVU (HIV/AIDS), saratani na utapiamlo.
Je mkanda wa jeshi huambukizwa?
Hapana ugonjwa huu hauambukizwi kutoka kwa mtu
mmoja kwenda kwa mwingine! Lakini iwapo itatokea mtoto au mtu mzima
ambaye hajawahi kupatwa na ugonjwa wa tetekuwanga maishani mwake na
ambaye pia hajawahi kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo akakutana na mtu
mwenye ugonjwa wa mkanda wa jeshi, mtoto au mtu huyo atapatwa na
ugonjwa tetekuwanga na siyo mkanda wa jeshi.
Dalili
Dalili ya awali kabisa ya mkanda wa jeshi ni
maumivu makali sehemu fulani/ upande mmoja wa mwili yakiambatana na hali
ya ganzi na hisia za kuungua kwenye ngozi. Maumivu pamoja na hisia za
kuungua huwa makali sana na hutokea kabla ya vipele/michubuko kutokea
kwenye ngozi.
Kawaida, vipele au michubuko huusisha eneo fulani
la mwili kuanzia kwenye uti wa mgongo kuzunguka kuelekea eneo la tumbo
au kifua. Michubuko pia inaweza kutokea kwenye maeneo yanayozunguka
uso, macho, mdomo au masikio.Dalili nyingine ni pamoja na :
• Maumivu ya tumbo
• Homa
• Maumivu ya mwili mzima
• Vidonda sehemu za siri
• Maumivu ya kichwa
• Maumivu ya viungo
• Kuvimba kwa mitoki/ matezi
Iwapo neva za maeneo ya uso zitaathiriwa, mgonjwa anaweza kupatwa na matatizo ya kuona, kuonja, au kusikia.
Vipimo
Ni nadra sana kufanya Vipimo maalum kwa ajili ya
utambuzi wa ugonjwa huu, isipokuwa kwa nchi zilizoendelea. Kwa ujumla
utambuzi wa ugonjwa huu hufanyika kwa kuchukua historia ya mgonjwa na
kuchunguza sehemu ya ngozi iliyoathiriwa.
Vipimo vya damu yaani FBP huonesha ongezeko la chembe nyeupe za damu na antibodies dhidi ya virus wa tetekuwanga.
Matibabu
Matibabu ya mkanda wa jeshi hujumuisha matumizi ya
dawa kama vile Acyclovir, Famciclovir na Valacyclovir kwa ajili ya
kuua virus wanaosababisha ugonwja huu. Dawa hizi husaidia kupunguza
maumivu, kuzuia madhara zaidi ya ugonjwa huu na kupunguza muda wa
ugonjwa.
Dawa hizi hutolewa angalau saa 72 baada ya mgonjwa
kuanza kuhisi maumivu na hali ya kuungua. Ni vema dawa zianze kutumika
kabla ya vipele/michubuko kujitokeza.
Jamii ya dawa za corticosteroids kama vile
prednisolone husaidia kupunguza maumivu na uvimbe kwa badhi ya wagonjwa.
Dawa nyingine zinazofaa kutumika ni pamoja na jamii ya antihistamines
kwa ajili ya kupunguza muwasho, dawa za maumivu, calamine lotion kwa
ajili ya kupunguza muwasho. Aidha mgonjwa anashauriwa kupata mapumziko
ya kutosha
Matarajio
Mkanda wa jeshi kwa kawaida huchukua kati ya wiki
mbili hadi tatu kupona wenyewe. Aidha ni nadra sana kwa ugonjwa huu
kujirudia tena. Iwapo neva zinazothibiti mwendo katika mwili zitakuwa
zimeathirika, mgonjwa anaweza kupatwa na kupooza kwa muda au kwa kudumu
kwa sehemu ya mwili iliyoathiriwa. Wakati mwingine, maumivu
yanayosababishwa na mkanda wa jeshi yanaweza kudumu kwa miezi mpaka
mwaka hata baada ya mgonjwa kupona kabisa. Maumivu haya yanayojulikana
kama postherpetic neuralgia kwa kawaida huwakumba wagonjwa wenye umri wa
zaidi ya miaka 60 na husababishwa na uharibifu katika neva za mwili.
Madhara
Madhara ya mkanda wa jeshi ni pamoja na kupatwa na
shambulio jingine la ugonjwa huu, maambukizi ya bakteria, upofu iwapo
eneo la jicho litahusika, ukiziwi, maambukizi katika utando wa ubongo
(encephalitis), uwepo wa vimelea kwenye damu (sepsis) au ugonjwa
unaoitwa Ramsay Hunt Syndrome iwapo utahusisha neva za uso.
Kinga
Epuka kabisa kugusa eneo lenye vipele au michubuko
kwa mtu mwenye mkanda wa jeshi au tetekuwanga iwapo hujawahi kuugua au
kupata chanjo ya tetekuwanga.
Ni vema kupata chanjo dhidi ya virus wa Varicella
zoster kama inapatikana katika nchi au eneo ulilopo . Tafiti zimeonesha
kuwa, watu wazima wanaopata chanjo hii wana uwezekano mdogo sana wa
kupata madhara ya mkanda wa jeshi kuliko wale wasiochanjwa.
IMETOKA Jamiiforums.com
No comments:
Post a Comment