Tukio hilo lilitokea juzi mchana kwenye sherehe ya
Kipaimara kwa mtoto Dickson Nungu (14) na kuzua hofu kubwa kwa wakazi
wa kijiji hicho ambao wanaonekana kutoamini kilichotokea.
Wingi wa wagonjwa hao umesababisha zahanati hiyo
kuelemewa na kiasi cha wengine kulazwa chini kwenye udongo, barazani na
kwenye miembe wakisubiri kupatiwa huduma ya kwanza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Mskhiela
alisema polisi inawashikilia watu watatu kuhusiana na tukio hilo na
vinywaji na mabaki ya chakula kilicholiwa vimezuiliwa huku sehemu
ikichukuliwa sampuli ili kupelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa uchunguzi zaidi.
Alisema waliopatiwa matibabu na kuruhusiwa ni watu
50 huku 190 wakiwa bado wanatibiwa Lyangweni na wengine 30 wakilazwa
Peramiho. Hata hivyo, Kamanda Mshkhiela alisema walioathirika
wanaendelea kuongezeka.
Mtoto Nungu, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la
sita katika Shule ya Msingi Litapwasi, alipata Kipaimara hicho na mara
baada ya chakula cha mchana, waalikwa walipewa pombe za kienyeji na
wengine togwa. Baada ya muda mfupi, waliokunywa togwa na chakula, kila
mmoja kwa wakati wake alianza kujisikia maumivu ya tumbo na kuharisha
mfululizo huku wengine wakitapika damu.
Mama mzazi wa kijana huyo, Philbeta Ngonyani (36),
ambaye pia amelazwa katika Hospitali ya Misheni Peramiho alisema:
“Nimefikishwa hospitalini jana (juzi) saa nane usiku nikiwa sijitambui
kutokana na maumivu makali kwa kuharisha mfululizo baada ya kunywa
togwa.”
Akielezea tukio hilo alisema, anakumbuka siku moja
kabla ya tukio, (Jumamosi iliyopita) yeye na wenzake (majirani)
walishirikiana kupika togwa na walianza kazi hiyo saa sita adhuhuri na
kumaliza saa 10 jioni na kisha kuiweka katika chumba kimoja ili ipoe
kisha walimkabidhi ufunguo wa chumba hicho mtu aliyemtaja kuwa ni jirani
yao, Ridhiwan Shawa ili siku ya sherehe mtu atakayehitaji kinywaji
ampatie.
Alisema, juzi mchana mara baada ya mwanaye kutoka
kanisani, waalikwa walifika nyumbani kwake wakiwa na watoto wao na
baadhi ya ndugu na jamaa zao kwa ajili ya kujumuika kumpongeza kijana
huyo na vyakula mbalimbali vilipikwa kama wali, pilau na ugali.
Alisema mara baada ya kula, vinywaji vilitolewa na
kijana wake na baadhi ya watu walipatiwa soda na wengine waliomba pombe
za kienyeji na togwa. “Waliokunywa pombe na soda hawakudhurika lakini
waliokunywa togwa wengi walianza kusikia maumivu ya tumbo na kuanza
kuharisha na kutapika mfululizo na wengine kuharisha damu, baadhi
walirudi nyumbani na wengine walikimbilia zahanati.”
Alisema yeye, mumewe Ines Nungu pamoja na kijana wao mwingine, Matson wanaumwa tumbo, kuharisha na kutapika.
Jirani ambaye pia amelazwa, Aloysia Ngonyani
alisema alifikishwa hospitalini hapo juzi usiku wa saa saba akiwa na
maumivu makali ya tumbo huku akihara na kutapika baada ya kunywa togwa. SOMA ZAIDI KUTOKA MWANANCHI.COM
No comments:
Post a Comment