Wednesday 3 September 2014

MADHARA NA JINSI YA KUJIKINGA NA UGONJWA WA KISUKARI

UGONJWA WA KISUKARI UNASABABISHWA NA NINI?
Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na UKOSEFU au UPUNGUFU wa chembechembe (HORMONE ) kwa jina la insulin Au kushindwa kufanya kazi mwilini.



JE UGONJWA HUU UNASABABISHWA NA KULA SUKARI NYINGI?
Kula sukari nyingi sio sababu ya ugonjwa kisukari. Lakini lazima tuseme kwamba kula sukari nyingi si nzuri kwa afya yako kwani utaongeza uzito na kuweza kuathiri uwezo wa mwili wako kujikinga na maradhi tofauti. Hivyo sukari tutumie lakini kwa uangalifu.

KUNA AINA NGAPI ZA UGONJWA HUU?
Kuna aina mbili. Aina ya kwanza (Type 1) ni ile ambayo mwili unakuwa hauna kabisa hizo chembe chembe za INSULIN. Hujitokeza mapema kabisa tangu katika umri mdogo wa utoto. Matibabu yake ni sindano za insulin kabla ya kula chakula na wakati tofauti katika siku nzima. Aina ya pili ni ile ambayo kuna upungufu wa insulin. Hivyo mwili una insulin ambayo haitoshi kwa mahitaji ya kila siku. Matibabu yake yanakwenda kwa awamu tofauti. Awamu ya kwanza ni kuepuka vyakula vya uwanga na sukari na kula vyakula kama mikate ya ngano nzima ili ile insulin kidogo iliyopo iweze kutosha. Iwapo hii haitosaidia kuna aina fulani za vidonge ambazo hupewa mgonjwa. Vidonge hivi husaidia kuongeza insulin kidogo iliyomo mwilini. Ikiwa hii pia haikusaidia hapo tena hubidi mgonjwa kusaidiwa kwa shindano za insulin. Aina ya 2 mara nyingi hujitokeza katika umri wa kati au umri mkubwa na sio katika umri wa watoto wadogo.

NINI KINACHOFANYA MTU KUWEZA KUPATA UGONJWA HUU:
Mara nyingi ni urithi katika ukoo, yaani asili ambayo wazee waliopita au kutangulia walikuwa nao ugonjwa huu. Lakini pia hitilafu fulani za mwili zinaweza kufanya ile insulin iliyomo mwilini kutokufanya kazi.

JEE MTU ATAJUWAJE KAMA ANA UGONJWA WA KISUKARI?
Dalili zifuatazo zinaweza kujitokeza: kwenda haja ndogo mara kwa mara, na kunywa maji kwa wingi ( kiu haishi). Pia wengine hupoteza uzito, kukaukwa na ngozi na pia kupata aina ya ngazi katika miguu. Wengine wanaweza kuwa na kidonda ambacho kinachelewa kupona katika sehemu yo yote ya mwili. Pia kupoteza hisia katika miguu au viganja inaweza kujitokeza.

NINI ATHARI ZA UGONJWA HUU?
Baada ya muda mrefu ugonjwa wa sukari huleta athari ya mishipa ya fahamu na kusababisha kupoteza hisia za ngozi na viganja au nyayo na kupungua nuru ya macho. Pia athari ya mafigo huweza kujitokeza na uzungukaji wa damu unaweza kupungua katika baadhi ya sehemu na kusababisha kufa kwa sehemu za mwili. Kujitokeza kwa dalili hizi kunategemea ni kiasi gani matibabu yamefanikiwa na wakati wa kuanza kwa matibabu hayo baada ya kujuilikana kwamba mtu ana ugonjwa huu.

VIPI UNAWEZA KUJIKINGA NA UGONJWA HUU?
Ikiwa unayo historia katika familia sio lazima kwamba utapata ugonjwa huu. Lakini kwa wale ambao wanaweza kuupata wanaweza kuuchelewesha kwa kujitahidi kuishi maisha ya afya nzuri kwa kula chakula bora, mazoezi, kula mboga mboga kwa wingi na kujiepusha na uzito wa mwili. Pia kupima damu baada ya kila muda ikiwa una historia katika ukoo au una wasi wasi kutokana na dalili zilizotajwa hapo juu.

JEE KUNA MATIBAU YA MARA MOJA KUONDOA UGONJWA HUU?
Kwa dawa za hospitali mpaka sasa hakuna dawa ya kuondoa moja kwa moja ingawa hasa kwa aina ya 2 watu baada ya kurekebisha vyakula wanaweza kujiweka katika hali hali ambayo mwili unaweza kutumia insulin yake kidogo bila ya kula vidonge au sindano. Kuna utafiti wa kufanya transplant ili kuongeza insulin mwilini kwa kutumia sehemu (pancreas) ya mtu mwengine lakini bado haujafanikiwa kuweza kutumika kama ni matibabu.

IMETOKA JAMII FORUM

No comments:

Post a Comment

.